|
MAZINGIRA
Nchi ya Tanzania, kama nchi nyingine nyingi duniani, imegawanyika katika sehemu zenye majira na mazingira tofauti. Tanzania, ambayo iko Afrika Mashariki, ina milima, mabonde, misitu, mito na maziwa.
Katika misitu na mabonde kuna miti ya aina mbalimbali kama mikaratusi, mipingo na kadhalika. Baadhi ya misitu na mabonde, kama yale ya sehemu mbalimbali mkoani Kilimanjaro, yamebarikiwa kuwa na rutuba nzuri, maporomoko ya maji, mito yenye maji safi na baridi, na chemchem zinazotiririka maji mwaka mzima.
Pia Tanzania imebarikiwa kuwa na mlima mrefu kuliko milima yote barani Afrika. Mlima huu, unaoitwa Kilimanjaro, una misitu mikubwa na kilele chake kina theluji. Kwa keli, mlima huu unavutia machoni.
Katika sehemu nyingine za Tanzania, kuna tambarare zenye rutuba nzuri na nyasi za aina mbalimbali. Mara nyingi, wananchi wengi hutumia sehemu hizi kwa kulisha mifugo yao, kulima mazao mbalimbali, au kufanya makazi yao. Serikali ya Tanzania inatilia sana mkazo suala la utunzaji wa mazingira yake. Hii ni rasilimali ambayo serikali inahakikisha kuwa inarithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
|