Home
Overview
Technical Help

Select Unit > Unit 9: Usafiri wa Majini > Lesson 5:

    

VYOMBO VYA USAFIRI WA MAJINI

Wakazi wa sehemu ya Tanzania Mashariki, na wale wanaoishi kando kando ya maziwa na mito mbalimbali, wanategemea sana usafiri wa majini. Njia hii ya usafiri imekuwa ikitumiwa tangu enzi za mababu, na katika sehemu nyingine ndiyo njia pekee ya usafiri. Kwa mfano, katika visiwa vidogo vidogo, ambako hakuna viwanja vya ndege, wakazi wa sehemu hizo hutumia usafiri wa majini kuingia na kutoka katika visiwa hivyo.

Katika sehemu hizi, wananchi hutumia vyombo vya aina mbalimbali vya kijadi kama ngarawa, mashua, mitumbwi, madau na majahazi. Mara nyingi vyombo hivi huwa vinatumia makasia na matanga katika uendeshaji wake. Hivyo, waendeshaji vyombo hivi hutegemea sana upepo na miendo ya mikondo ya maji katika kuendesha vyombo hivi. Mara nyingi vyombo hivi huwa na mwendo wa taratibu sana. Waendeshaji wengi wa vyombo hivi wana ujuzi na uzoefu ambao mara nyingi huwa unarithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Pamoja na vyombo vya kijadi, siku hizi pia wananchi wanatumia boti za kisasa zinazoendeshwa kwa mashine zinazotumia mafuta ya petroli. vyombo hivi vya kisasa huwa vina mwendo wa kasi na huwa havitegemei upepo au mwendo wa mikondo ya maji katika uendeshaji wake.

© African Studies Institute, University of Georgia