Mji wa Malindi
Sasa
tuko mjini Malindi. Mji wa Malindi uko pwani kaskazini ya
mji wa Mombasa huko Kenya. Ni mashuhuri kwa
pwani yake yenye mchanga safi. Karibu sana na ufuko kuna mahoteli
mengi na nyumba za wageni wanaoitembelea Kenya. Nyumba za wageni
ni vibanda vidogo ambavyo vimejengwa kwa mawe ya Mtiwa baharini
na kupakwa chokaa nyeupe.
Paa zimeezekwa kwa makuti yaani
majani ya mnazi.
Kuna baraza ndogo
mbele ya nyumba na watu hupenda kukaa wakati wa jioni kupunga
upepo baridi kutoka pwani.
Nyumba za wageni na mahoteli yamezungukwa na maua na miti ya minazi iletayo upepo wa kuburudisha. Sehemu hii ni joto sana. Kwa hivyo upepo wa baridi unaosababishwa na miti hii unawaburudisha sana. Kuta za hoteli hupambwa kwa kanga ambazo zimetengenezwa na wenyeji katika viwanda vya Kenya. Kanga hizi huonyesha utamaduni wa wenyeji wa sehemu hizi. Utamaduni huu husisitizwa pia katika sanaa zinazoonekana ukutani, viti na meza katika sehemu mbali mbali za hoteli. Taa, milango na madirisha yaliyopambwa kwa nakshi mbali mbali.
Miti ya minazi ina faida nyingi. Huleta kivuli na majani yake hutumiwa kuezekea paa za nyumba na matunda yake hutumika kwa namna mbali mbali. Nazi changa huitwa madafu na maji yake hutumiwa kama kinywaji baridi wakati wa jua kali. Maji ya nazi kavu hutumiwa kupikia vyakula mbali mbali.
|