Kupanda Mlima Kilimanjaro
Mlima Kilimanjaro, katika nchi ya Tanzania, ni maarufu dunia nzima kutokana na urefu wake. Ni mlima mrefu kuliko yote Afrika, futi 19,430, na wa pili katika dunia nzima. Kilele chake kina theluji mwaka mzima na huwavutia watalii wengi ambao hupenda kuupanda mlima huu kama namna ya kujistarehesha. Mtalii anaweza kupanda wakati wo wote wa mwaka lakini nyakati nzuri ni kuanzia mwezi Juni hadi Oktoba na kuanzia Desemba hadi Februari.
Ingawa kuna
njia mbalimbali za kukifikia kilele cha mlima huu, watalii wengi hupendelea kuchukua
njia ya Marangu, njia aliyoitumia mpandaji wa
kwanza aliyekifikia kilele hicho. Mtu ye yote, mzee au kijana anaweza kuupanda
mlima huu kupitia njia ya Marangu kwa sababu mtelemko wake
sio mkali.
Njiani anaweza kuona mandhari ya
aina mbalimbali ambayo huhifadhiwa na serikali ya Tanzania, kitengo cha Utalii.
Kufikia kilele, mpandaji anaweza kuchukua siku tano au sita. Wengi hushauriwa kuchukua siku sita. Kwa kawaida inachukua siku tatu kupanda mpaka kileleni na siku mbili kushuka mpaka kituo cha kuanzia safari. Ikiwa mpandaji atachagua kutumia siku sita badala ya tano, anaweza kutumia siku nzima ya mapumziko kabla ya hatua za mwisho za kukifikia kilele. Wapandaji wengi ambao wanatumia siku sita badala ya tano hujiongezea uwezekano mkubwa zaidi wa kufika kileleni kuliko wale ambao wanatumia siku tano tu. Hii ni kwa sababu uchovu wa siku ya tano unakuwa kizingiti kikubwa kwa wapandaji kumaliza safari mpaka kileleni. Kuna vibanda na mahema ambayo wapandaji wanaweza kutumia kupumzika na kulala wakati wa usiku. Pia kuna wataalamu wanaowasaidia wapandaji kubeba mizigo yao, kuwapikia vyakula muhimu, na kuwaongoza njia zifaazo kufikia vituo vya mapumziko na hata njia nzima mpaka kileleni.
|